Daktari wa Yanga Moses Etutu amesema timu inaendelea na maandalizi kuelekea mchezo wa mkondo wa kwanza kuwania tiketi ya kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya Silver Strikers ambao utapigwa Jumamosi, Oktoba 18 huko Malawi
Etutu amesema wachezaji wote ambao hawakuwa na majukumu ya timu za Taifa wanaendelea na maandalizi chini ya kocha mkuu Romain Folz anayesaidiana na Patrick Mabedi
Akimzungumzia mshambuliaji Clement Mzize ambaye alikuwa majeruhi, Etutu amesema nae amerejea mazoezini ingawa bado hayuko tayari kwa asilimia 100
"Wachezaji wote wanaendelea na maandalizi kuelekea mchezo wetu wa ligi ya mabingwa dhidi ya Silver Strikers ambao utapigwa mwishoni mwa wiki nchini Malawi"
"Tumekuwa na wakati mzuri wa kufanya maandalizi, habari njema ni kuwa kwa sasa hatuna majeruhi, Clement Mzize ambaye alikuwa nje akisumbuliwa na changamoto ya maumivu ya nyama za paja nae amerejea kikosini"
"Ameanza kushiriki mazoezi na timu ingawa anaweza kuhitaji muda zaidi ili kuwa fiti kwa asilimia 100, sasa naweza kusema yuko kwenye asilimia 70"
"Lakini bado tuna siku chache kuelekea mchezo wetu dhidi ya Silver Strikers, anaweza kuwa tayari kutumika kwenye mchezo huo,"alisema Etutu
Katika hatua nyingine, baadhi ya wachezaji ambao walikuwa kwenye majukumu ya timu za Taifa tayari wamerejea
Viungo washambuliaji Ecua Celestin na Lassine Kouma wamerejea mapema baada ya kukamilisha majukumu yao timu ya Taifa ya Chad. Wachezaji wengine wanatarajiwa kurejea leo
Yanga inatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam kesho Alhamisi kuelekea Malawi tayari kwa mchezo dhidi ya Silver Strikers ambao utapigwa siku ya Jumamosi