Baada ya kutangazwa kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Kocha Patrick Mabedi leo ameanza rasmi majukumu yake katika maandalizi kuelekea mchezo wa mkondo wa pili kuwania tiketi ya kutinga makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa (CAFCL) dhidi ya Silver Strikers
Baada ya kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza dhidi ya Silver Strikers jana, leo Yanga imerejea mazoezini ambapo wachezaji walifanya program maalum ya 'recovery' kwa wachezaji waliotumika jana huku wengine wakifanya mazoezi ya kawaida
Meneja wa Yanga Walter Harrison amesema leo na kesho asubuhi watajifua huko Malawi kabla ya kuanza safari ya kurejea Tanzania siku ya kesho jioni
"Program ya mazoezi inaendelea vizuri kama tulivyozungumza jana baada ya mchezo kila kitu kimebadilika, tunarejea Tanzania kesho jioni, saa 10 na tutafika Dar es salaam majira ya saa 2 usiku"
"Baada ya kutua Dar siku ya Jumanne tutaingia rasmi kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa marudiano utakaopigwa Jumamosi Oktoba 25 uwanja wa Benjamin Mkapa"
"Nisema tu kila kitu kinaendelea vizuri chini ya chini ya kocha Patrick Mabedi na tunaamini tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuweza kujiandaa kuelekea mchezo wa marudiano," alisema Harrison
Aidha Harrison aliwahakikishia mashabiki wa Yanga kuwa timu inafanya maandalizi kabambe ili kuhakikisha wanashinda mchezo wa marudiano na kufuzu hatua ya makundi