Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo, amesema uongozi umejipanga na watampa sapoti kocha Patrick Mabedi kuelekea mchezo wa mkondo wa pili kuwania kufuzu hatua ya makundi ligi ya mabingwa dhidi ya Silver Strikers utakaopigwa Jumamosi ili kufuzu kwa hatua ya makundi.
Yanga baada ya kurejea nchini juzi Jumatatu, jana Jumanne mchana kikosi kilingia kambini kuanza maandalizi ya mechi hiyo itakayopigwa Jumamosi Oktoba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 11:00 jioni.
Yanga itahitaji ushindi wa tofauti ya mabao angalau 2-0 ili kuikomboa tiketi ya kwenda makundi kwa msimu wa nne mfululizo kwenye mashindano ya CAF.
Gumbo alisema mbali na kukutana na Mabedi ambaye ni raia wa Malawi, watakutana pia na wachezaji wao kuwaongezea morali kwenye maandalizi yao na hata mechi hiyo.
Bosi huyo aliongeza kuwa, wana imani kubwa kwamba licha ya mabadiliko ya benchi la ufundi kufuatia kumfuta kazi aliyekuwa kocha mkuu, Romain Folz, lakini wana kikosi imara ambacho kinaweza kubadili matokeo hayo.
“Huu ni mchezo muhimu dhidi ya Silver Strikers, nataka kukwambia maandalizi ya mchezo huu sio ya kawaida, ni kama tunakwenda kucheza fainali, unaona ambavyo tumewahi kuingia kambini, hatuna muda wa kupoteza,” Gumbo amenukuliwa na Mwanaspoti.
“Uongozi wetu utakwenda kambini, tutazungumza na kocha atatueleza kama kuna kitu anahitaji ili akipate kwa haraka na baada ya hapo tutakutana na wachezaji wa timu nzima, tunataka kuhakikisha saikokolojia yao inakuwa ni kuhusu kushinda kikubwa."
“Kupitia chombo chako wafikishieni salamu mashabiki wetu kwamba tupo timamu na wao wajipange, hii ni mechi yetu waje uwanjani lakini tuna jukumu la kushirikiana kurudisha heshima yetu, haitakubalika tushindwe kufuzu mara mbili mfululizo hatua ya makundi."