Kocha Msaidizi wa Yanga Patrick Mabedi amesema anaamini mshambuliaji Prince Dube yuko katika kipindi cha mpito na kuwa ni suala la muda tu atakuwa sawa.
Mabedi amesema anatambua Dube anakabiliwa na presha kubwa hasa kwa kuwa hajafanya vyema katika mechi chache zilizopita
"Dube amefanya mambo mengi mazuri. Nafahamu ana mzigo mkubwa mabegani mwake. Kwa uwezo alionao atakaa sawa."
"Kuna presha nyuma yake lakini hiyo kawaida kwa wachezaji wakubwa popote pale. Usipofunga lazima maswali yawe mengi. Ni suala la muda Dube atarejea kwenye makali yake sina wasiwasi," alisema Mabedi
Akizungumzia maandalizi kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar ambao utapigwa kesho Jumanne katika uwanja wa KMC Complex, Mabedi amesema walifanya vyema katika mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Silver Strikers, dhamira yao ni kuendeleza kasi hiyo
Mabedi amesema wamefanyia kazi eneo la matumizi ya nafasi ili kuhakikisha wanaongeza ufanisi mbele ya lango
"Nina furaha na namna Wachezaji wetu walivyocheza dhidi ya Silver Striker. Kama Kocha napaswa kuona timu yetu ikicheza vizuri, nadhani muda unavyozidi kusogea mbele kimbinu tutakuwa imara zaidi"
"Kila mchezo una ugumu wake, kwenye ligi lazima ushindani uwepo na tunaheshimu kila mpinzani. Tunahitaji kuwa makini sana kwenye mchezo wa hapo kesho dhidi ya Mtibwa. Tunachokifanyia kazi mazoezini kwa sasa ni kuhakikisha Wachezaji wanatumia vyema kila nafasi wanayoipata"
"Mchezo wa mwisho mashabiki walijitokeza kwa wingi sana. Niwapongeze sana mashabiki waliotoa muda wao kuja kuungana nasi. Ni matarajio yetu kuwaona kwa wingi hapo kesho kwa lengo la kuwapa Wachezaji wetu hamasa," aliongeza Mabedi