Mshambuliaji wa Yanga Clement Mzize amefanyiwa upasuaji wa goti ambao unatarajiwa kumuweka nje kwa miezi miwili.
Mzize alipata majeraha kwa mara ya kwanza wakati akiwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa katika michuano ya CHAN 2024 iliyofanyika mwezi August mwaka huu.
Baada ya kupona majeraha hayo, Mzize alirejea dimbani mwanzoni mwa msimu akicheza mechi ya Ngao ya Jamii na hatua ya awali ligi ya mabingwa dhidi ya Wiliete Sc mchezo wa kwanza uliopigwa Angola.
Hata hivyo alitonesha majeraha katika mchezo huo na kuwa nje kwa takribani wiki tatu. Siku moja kabla ya mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Silver Strikers, Mzize aliyekuwa tayari ameanza mazoezi na timu, akaumia tena.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe kuwa Mzize anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa wiki 8-10 na hivyo atakosa mechi za awali hatua ya makundi CAFCL na pengine michuano ya AFCON 2025 inayotarajiwa kufanyika mwezi ujao nchini Morocco.
"Mara ya mwisho tuliwajulisha kuhusu hali ya majeraha ya mchezaji Clement Mzize. Baada ya ushauri wa jopo la madaktari wakishirikiana na benchi la Ufundi na Mchezaji mwenyewe tulikubaliana afanyiwe upasuaji."
"Maamuzi haya yalikuja baada ya kuona anaendelea kupata maumivu kwenye goti lake kila alipokuwa akirejea uwanjani. Nipende kuutangazia Umma kuwa, mchezaji Clement Mzize atakuwa nje ya uwanja kwa wiki nane mpaka kumi," alisema Kamwe.