Kikosi cha Yanga leo kinaelekea visiwani Zanzibar kukamilisha maandalizi kabla ya mchezo wa kwanza wa makundi ligi ya mabingwa dhidi ya AS FAR utakaopigwa Jumamosi, Novemba 22 katika uwanja wa New Amaan Complex.
Wakati Yanga wakielekea Zanzibar leo, wapinzani wao AS FAR wamethibitisha kuwa watawasili Zanzibar siku ya kesho Jumatano, majira ya saa 3 usiku.
Wananchi wanakwenda Zanzibar huku wakiwa na dhamira moja tu, kushinda mchezo dhidi ya AS FAR kuanza vyema kampeni ya kuisaka robo fainali ya pili katika ligi ya mabingwa.
Tayari viingilio vya mchezo huo vimewekwa hadharani Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe akiwataka mashabiki wa timu hiyo visiwani Zanzibar kununua tiketi zao mapema na kuhakikisha wanaujaza uwanja wa New Amaan Complex.
