Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe ameonesha kushangazwa na wanaohoji sababu za mshambuliaji Clement Mzize kutosafiri Morocco kupokea tuzo yake ya goli bora la msimu 2024/25 katika mashindano ya CAF.
Kamwe amefafanua kuwa haukuwa uamuzi wa Mzize peke yake bali ni baada ya ushauri uliotolewa na madaktari waliomfanyia upasuaji wa goti hivi karibuni.
Kamwe amesema uongozi wa Yanga uliwasilisha mapema kwa CAF juu ya hali ya mchezaji huyo na ndio maana alitakiwa kurekodi ujumbe maalum wa shukrani ambao ulichezwa baada ya kutangazwa ni mshindi.
"Hili sio jambo ambalo Yanga iliamua yenyewe, Mzize alitutaarifu juu ya ushauri ambao amepewa na daktari kuwa sio vyema kusafiri kwenda Rabat, Morocco kutokana na upasuaji ambao amefanyiwa hivi karibuni."
"Sisi tukawasiliana na CAF ambao pia walihitaji kupata hiyo ripoti ya daktari lakini pia waliwasiliana na madaktari na kuthibitisha. Ndio maana hata baada ya Mzize kutangazwa mshindi, MC alisikika akisema Mzize ametoka kufanyiwa upasuaji hivyo ameshindwa kusafiri."
"Maana yake taarifa walikuwa nayo kuhusu Mzize na kama ingekuwa taarifa ya uongo au yenye utata wasingeweza kuifanya kuwa rasmi na kutangaza kwenye tukio kubwa kama lile," alisema Kamwe