Kocha wa timu ya AS FAR Alexandre Santos amekiri haikuwa rahisi kwao kukabiliana na kiungo mshambuliaji wa Yanga Pacome Zouzoua ambaye ni kama aliwakodi mabeki wa timu hiyo katika mchezo wa ligi ya mabingwa uliozikutanisha timu hizo mwishoni mwa wiki Yanga ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 uwanja wa New Amaan Complex.
AS FAR ambao walitua Zanzibar wakijiamini, walijikutana wakikutana na kipigo cha kwanza msimu huu huku Santos akikiri Pacome aliwalaza na viatu.
“Yanga wana wachezaji wengi wazuri lakini yule namba 10 (Pacome) ni mchezaji hatari zaidi. Ana ubunifu sana mpira ukiwa kwenye miguu yake, kuna wakati timu yake ilienda chini lakini akairudisha mchezoni, ni mchezaji mwenye kiwango kikubwa sana".
“Baada ya kumuona kipindi cha kwanza, tukajipanga kumtuliza kipindi cha pili, lakini bado alifungua sana ukuta wetu, nadhani hali ya hewa nayo iliwasumbua wachezaji wangu,” alisema Santos baada ya dakika 90 za moto dimba la New Amaan Complex.
Yanga imechafua rekodi ya AS FAR msimu huu kwani mara ya mwisho kupoteza ndani ya dakika 90 ilikuwa Mei 3 mwaka huu ilipocharazwa 2-1 ugenini dhidi ya Wydad Athletic kwenye Ligi ya Morocco na kipigo ch Yanga kimesitisha safari ya kutofungwa mechi 19 za mashindano yote.
Far Rabat inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Morocco maarufu Botola Pro 1, hadi sasa imefunga jumla ya mabao 22 na yenyewe kufungwa manne likiwamo la Dube.
Wakati Yanga ikisafiri Algeria kuikabili JS Kabylie kwenye mchezo wa pili wa makundi siku ya Ijumaa, AS FAR watakuwa nyumbani kuikabili Al Ahly ambayo kwenye mchezo wa kwanza iliichapa JS Kabylie mabao 4-1