Kwa mujibu wa mapendekezo ya maboresho yaliyotolewa na mkufunzi wa Yanga Pedro Goncalves, eneo la kiungo mkabaji ni miongoni mwa maeneo ambayo kocha huyo raia wa Ureno amehitaji kuimarishwa.
Licha ya usajili wake kutikisa katika dirisha lililopita, kiungo Moussa Balla Conte bado hajaweza kulishawishi benchi la ufundi na sasa inaelezwa Yanga imejipanga kurudi sokoni kusaka mbadala wake.
Rais wa Yanga Injinia Hersi Said anampigia hesabu kali kiungo wa Azam Fc raia wa Ghana, James Akaminko.
Hii haitakuwa mara ya kwanza Yanga kujaribu kumnasa Akaminko ambaye bado ana mkataba na Azam Fc ambao utafika tamati mwishoni mwa msimu.
Wakati wa sakata la usajili wa Feisal Salum kwenda Azam Fc, Yanga ilituma ofa kuwataka Akaminko na Kipre Junior ambaye kwa sasa anaitumikia klabu ya MC Alger.
Kwa nyakati zote Azam Fc haijawa tayari kumuachia Akaminko lakini wakati huu mambo yanaweza kuwa tofauti kwa kuwa mchezaji mwenyewe yuko tayari kuondoka kutokana na ufinyu wa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
Akiwa na mkataba wa chini ya miezi sita, Akaminko anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine na hata kusaini mkataba wa awali kama makubaliano yanafikiwa.
Mtihani utabaki kwa Azam Fc wamuuze sasa au aondoke bure pale mkataba wake utakapomalizika.