Yanga leo inakamilisha maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Azam FC, utakaopigwa kesho Jumanne, Januari 13, katika Uwanja wa Gombani, Pemba.
Habari njema kwa mashabiki wa Yanga ni kurejea kwa nyota wao waliokuwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ambao tayari wametua Zanzibar na wako tayari kutumika kwenye mchezo huo muhimu.
Mabeki Bakari Nondo Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Dickson Job na Mohamed Hussein walikuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars kilichoweka historia ya kufuzu hadi hatua ya 16 bora katika michuano ya Afcon 2025 inayoendelea nchini Morocco.
Juzi, nyota hao waliungana na wenzao wa Taifa Stars walipoalikwa Ikulu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hafla maalumu ya kuwapongeza kwa mafanikio hayo ya kihistoria.
Baada ya tukio hilo, wachezaji hao sasa wamejiunga rasmi na kikosi cha Yanga na wako tayari kuendelea na majukumu yao, huku kocha Pedro Gonçalves akipata chaguo pana zaidi kuelekea pambano la fainali dhidi ya Azam FC.