Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mashujaa Fc ambao utapigwa kesho Jumatatu katika uwanja wa KMC Complex.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo Pedro amesema anatambua uimara wa Mashujaa Fc hasa safu yao ya ulinzi ambayo imeruhusu mabao manne tu msimu huu.
Hata hivyo amesema Yanga iko tayari kukabiliana na mazingira yoyote katika mchezo huo lengo likiwa kuibuka na ushindi.
"Tunapoangalia msimamo wa ligi tunaoona mashujaa ikiwa timu nzuri, kwenye mechi 9 wameruhusu magoli manne tu, inaonesha ni timu imara inayoweza kujilinda, kwetu sisi ni changamoto nzuri kukutana na timu ya aina hii na tutautazamia kwa umakini ili kufanya vizuri".
"Wana wachezaji wazuri pia hata kwenye kushambulia hivyo tunatarajia mchezo mzuri kesho, kazi yetu ni kuifuata falsafa ya Yanga, Kucheza vizuri na Kushinda, tunaamini tumejiandaa vizuri na tutafanya vizuri," alisema Pedro.
Kocha huyo raia wa Ureno mewapongeza mashabiki wa Yanga kwa nguvu yao na sapoti wanayoipa timu yao nyakati zote akiwataka kujitokeza kwa wingi kuihamasisha timu yao katika mchezo huo ambao wanazihitaji alama zote tatu.
"Kwanza kabisa nina furaha kubwa kila ninapowaona Wananchi Uwanjani, niwapongeze sana kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuisapoti timu yao, Niwaombe pia waje kutusapoti Kesho kwenye mchezo wetu dhidi ya Mashujaa, Nina imani watafurahi," aliongeza Pedro