Mechi ya watani wa jadi, Yanga dhidi ya Simba maarufu Kariakoo Dabi iliyopangwa kufanyika Machi 1, 2026, itachezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Hayo yamesemwa na Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe ambao ni wenyeji wa mechi hiyo ikiwa ni ya mzunguko wa kwanza katika Ligi Kuu Bara.
Kamwe alitoa kauli hiyo baada ya kumalizika kwa mchezo wa ligi ya mabingwa kati ya Yanga dhid ya JS Kabylie Wananchi wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Kamwe ameandika:
"Mchezo wetu wa Ligi Kuu Machi 1, 2026 dhidi ya Simba SC, 'Kariakoo Derby' utapigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex saa 2:15 Usiku. Karibuni sana."
Kwa mujibu wa ratiba iliyofanyiwa maboresho na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), kisha kutangazwa Novemba 17, 2025, mechi hiyo namba 54, ilipangwa kufanyika saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, lakini sasa wenyeji Yanga wameipeleka Zanzibar.