Kocha Mkuu wa Yanga SC, Pedro Goncalves anasema tangu ametua Jangwani wamecheza mechi kadhaa kubwa, lakini kesho wanakwenda kukutana na mpinzani wao mkuu, klabu ya Simba.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo, Goncalves amesema amekiandaa kikosi chake kikamilifu kwenda kucheza na Simba kama timu na matarajio yake ni kuwa wachezaji wake watatekeleza kwa ufanisi kile walichokiandaa kwenye uwanja wa mazoezi ili kuibuka na ushindi.
"Tumeanza maandalizi tangu juzi na leo tunakwenda kumalizia maandalizi hayo, wachezaji wangu wapo tayari na wana morali ya kucheza mechi hii kubwa, kama kila kitu kitaenda sawa nina imani tutakwenda kufanya vizuri kesho"
"Hii ndiyo derby yangu ya kwanza dhidi ya Simba. Kazi yetu ni kujiandaa kwa ajili ya kushinda kila mechi tunayocheza. Iwe ni dhidi ya Cosmopolitan au Al Ahly, lengo letu siku zote ni ushindi."
"Ndivyo ilivyo hata kwa mchezo wa kesho; tunalenga kushinda, japokuwa tunatambua kwamba tunakwenda kukutana na mpinzani mwenye uwezo mkubwa."
"Simba ni miongoni mwa timu bora nchini Tanzania. Wamewekeza kwa kiasi kikubwa katika soka na, kwa maoni yangu, wamekuwa imara pia katika michuano ya kimataifa hivyo tunatarajia kucheza dhidi ya moja ya timu kubwa barani Afrika."
"Tunapaswa kuwa waangalifu na kujitolea kwa hali ya juu na kuonyesha umakini mkubwa ili tuweze kupata matokeo mazuri," alisema
Akizungumzia kuhusu kiungo mshambuliaji Pacome Zouazoua, Goncalves amesema baada ya mazoezi ya mwisho leo, itafahamika kama ataweza kutumika kwenye mchezo wa kesho.
"Kuhusu mchezaji Pacome, ni kweli kwamba ana majeraha. Sote tulishuhudia alipoyapata katika mchezo wetu dhidi ya JS Kabylie. Kwa sasa tunaendelea kufuatilia kwa karibu hali yake kiafya na baada ya mazoezi ya mwisho ya leo tutajiridhisha iwapo atakuwa tayari na sehemu ya kikosi kwa ajili ya mchezo wa kesho"