Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amekiri kuwa hawakuwa bora kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba uliopigwa uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar jana na kumalizika kwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana.
Kamwe amempongeza mlinda lango Djigui Diarra kwa kuiweka Yanga mchezoni kwa dakika zote 90 na kufanikiwa kuondoka na alama moja muhimu inayowafanya kuwa mbele kwa tofauti ya alama tano dhidi ya wapinzani wao Simba.
"Nawapongeza Simba wamecheza vizuri, walikuwa na nafasi ya kushinda mechi hii lakini sisi tulikuwa na mchezaji mkubwa langoni Djigu Diarra ametusaidia kupata alama moja."
"Mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo huu benchi la ufundi limeyaona na yanakwenda kufanyiwa kazi kwenye uwanja wa mazoezi."
"Ligi bado ni ndefu, ni mchezo wa 11, leo tumepata alama moja tofauti ya pointi kati yenu na wao ni tano tunaendelea na ligi."
"Ifahamike mwisho wa msimu atakayekumbukwa hapa ni bingwa na sio nani aliyeshinda dabi, leo tumepata pointi moja na muhimu tofauti na point kati yetu ni tano," alisema Kamwe.
Mchezo unaofuata kwa Yanga ni dhidi ya Singida BS ukitarajiwa kupigwa March 05 katika uwanja wa Airtel huko Singida.