Licha ya kukiri kuwa timu yake inakabiliwa na mechi mfululizo, kocha mkuu wa Yanga Pedro Goncalves amesema wako tayari kuikabili Singida BS katika mchezo wa ligi kuu utakaopigwa kesho Alhamisi, uwanja wa Airtel huko Singida.
Goncalves amesema wamekuwa na ratiba ngumu, kesho watacheza mechi ya tano katika kipindi cha wiki mbili, lakini wamejipanga kukabiliana na ratiba hiyo.
"Kwetu sisi kila mechi ni muhimu na sasa tunapita kipindi kigumu cha kucheza mechi mfululizo. Ukiangalia mechi ya kesho ni ya tano katika kipindi cha siku 15, mechi hizo pia zikihusisha kusafiri."
"Pamoja na changamoto hiyo, wachezaji wangu wanafahamu umuhimu wa kila mchezo. Tunahitaji kulinda nafasi yetu juu ya msimamo wa ligi."
"Tunafahamu tunakwenda kucheza na miongoni mwa timu bora ligi kuu ya NBC, nasi tumekuja hapa kucheza soka la ushindani tukihitaji kupata ushindi."
Aidha Goncalves amethibitisha kuwa beki Dickson Job alipata majeraha ya goti kwenye mchezo dhidi ya Simba na kuenda akawa nje ya uwanja kwa muda wa wiki nane.
Goncalves pia amesema kiungo Pacome Zouzoua atakosekana katika mchezo huo ingawa yuko karibu kurejea kikosini.
"Job alipata shida kubwa kwenye goti, yalikuwa ni majeraha mabaya ambayo yanaweza kumuweka nje kwa miezi miwili"
"Pacome atakosekana lakini nadhani yuko karibu kurejea, Edmund John nae bado anaendelea na matibabu baada ya changamoto ya bega"