Unaambiwa kiungo wa Yanga Mohamed Doumbia ambaye anacheza kwa mkopo klabu ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini, ni mmoja wa wachezaji tegemeo wa timu hiyo.
Tangu asajiliwe na timu hiyo kwenye usajili wa dirisha dogo, Doumbia amecheza kila mechi huku akifanikiwa kufunga bao moja.
Kuna uwezekano mkubwa nyota huyo akarejeshwa kikosini mwishoni mwa msimu pale muda wake wa mkopo utakapomalizika.
Ikumbukwe Yanga iliwatoa kwa mkopo nyota wake watatu wa kigeni Doumbia, Ecua Celestin na Moussa Balla Conte mikopo yao ikiwa ni miezi sita.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema uongozi unafuatilia maendeleo ya wachezaji hao na endapo wataonekana kufanya vyema, milango ya kurudi Yanga iko wazi.
“Tunafuatilia kwa ukaribu maendeleo ya hao wachezaji. Watathmini wetu wa video wanawafuatilia kuangalia viwango vyao na kwa mechi ambazo wanacheza tumekuwa tukitazama. Tumekuwa tukiwasiliana hizo timu kupata viwango vya utimamu ili kupata maendeleo yao."
“Baada ya msimu kumalizika, benchi la ufundi ndio litatoa tathmini ya jumla juu ya nafasi ya kila mmoja kama anarudishwa au la,” alisema Kamwe.
Doumbia ndiye anayeonekana kufanya vyema zaidi wakati Ecua ameanza kwa kusuasua JS Kabylie mara nyingi akitumika akitokea benchi wakati Conte anayeitumikia Raja CA, amecheza kwa takribani dakika 30 tu katika mechi 7 zilizopita