Kesho Jumapili March 15 Yanga itashuka uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Azam Fc katika mwendelezo wa ligi kuu ya NBC
Hii ni mechi muhimu sana kwa Yanga ambapo matokeo ya ushindi yatawaweka Wananchi kwenye nafasi nzuri katika mbio za kuwania ubingwa wa ligi kuu.
Msimu huu Azam Fc imejipambanua kuutaka ubingwa, ni wao na Yanga pekee ambazo hawajapoteza mchezo mpaka sasa lakini Azam Fc wakitoka sare mechi 6 huku Yanga ikitoka sare mechi mbili tu.
Habari njema kwa mashabiki wa Yanga ni kuwa katika mchezo huo huenda wakamshuhudia kiungo mshambuliaji Pacome Zouzoua akiterejea kikosini baada ya kukosekana kwa takribani wiki nne.
Pacome alipata changamoto ya bega kwenye mchezo wa kuhitimisha hatua ya makundi ligi ya mabingwa dhidi ya JS Kabylie, maumivu yaliyomuweka nje tangu wakati huo.
Tayari nyota huyo raia wa Ivory Coast amerejea kikosini licha ya kukosekana katika mechi zilizopita, kesho anaweza kuwa silaha muhimu ya Yanga.
Yanga leo inatarajiwa kukamilisha maandalizi yake katika uwanja wa Benjamin Mkapa kuelekea mchezo huo ambao utapigwa saa 2:30 usiku.
Kwa misimu ya karibuni mechi kati ya Yanga dhidi ya Azam Fc maarufu dabi ya Dar es salaam, inaonekana kuwa na ushindani zaidi pengine kuliko dabi ya Kariakoo.
Katika mechi mbili ambazo Yanga walipoteza kwenye ligi msimu uliopita, moja ilikuwa dhidi ya Azam Fc ikiwa mechi ya mkondo wa kwanza huku Yanga wakishinda mechi ya mkondo wa pili.