Msimu huu unaweza kusema Yanga ni kama ilicheza 'kamali' kwenye dirisha la usajili kwani nyota wengi waliosajiliwa na mabingwa hao wa kihistoria Tanzania Bara, wameshindwa kudhihirisha ubora wao.
Usajili wa nyota hasa wa kigeni kwenye dirisha kubwa haukulipa ambapo Yanga ililazimika kuwatoa kwa mkopo baadhi yao kwenye dirisha dogo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe juzi akabainisha kuwa usajili wa mwaka huu haukusimamiwa kwa asilimia 100 na Rais wa Yanga Injinia Hersi Said.
Kamwe alisema mapendekezo ya makocha ndio yaliyozingatiwa zaidi na pengine hatua hiyo imepelekea changamoto iliyojitokeza kwa baadhi ya wachezaji kuwa chini ya kiwango kuliko wale waliowakuta.
Sasa inaelezwa katika usajili ujao, Injinia Hersi atarejea kusimamia mchakato mzima na anatarajiwa kuanza na jaribio la kumrejesha kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki ambaye kwa sasa anaitumikia Al-Ittihad Tripoli nchini Libya.
Aziz Ki ni mchezaji aliyewahi kuwa kiungo muhimu sana kwa Yanga, akisaidia klabu kushinda mataji yote ya ndani, akitwaa tuzo ya mfungaji bora na mchezaji bora 'MVP'.
Alijiunga na Yanga mwaka 2022 na kutimiza mafanikio makubwa kabla ya kuhamia Wydad Athletic Club mwaka 2025. Baadaye alikamilisha uhamisho kwenda Al-Ittihad Tripoli mwezi Januari, 2026.
Vyanzo vya habari vinavyohusiana na uhamisho vimeripoti kuwa Yanga imeanza mchakato wa kumrudisha Aziz Ki kwenye kikosi chake kwa dirisha la usajili lijalo, wakizingatia mchango alioutoa nyakati zake za awali na uzoefu wake wa soka la Afrika.
Ripoti pia zinaonyesha kuwa mchezaji mwenyewe anataka kurejea Tanzania kuungana na familia yake, pia akikumbuka mahusiano yake mazuri na Yanga.
Licha kuondoka Yanga, Aziz Ki amekuwa akiifuatilia Yanga ambapo kwenye mitandao ya kijamii ameonekana kuchangia mijadala mbalimbali huku akiitakia kheri Yanga kwenye mechi zake wakati wa michuano ya ligi ya mabingwa na hata mchezo wa dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba.
Tangu kuondoka kwa Aziz Ki, eneo la kiungo cha ushambuliaji bado linayumba. Licha ya kumsajili Mganda Allan Okello, lakini mara nyingi kocha Pedro Goncalves amemtumia zaidi kama winga huku eneo hilo akiwatumia Mudathir Yahya, Maxi Nzengeli na hata Duke Abuya kwa nyakati tofauti.
Pengine hiyo ndio sababu kwa Yanga kufikiria kumrejesha Aziz Ki ambaye kwake pia Yanga ndio klabu iliyompaisha zaidi barani Afrika.