Kocha raia wa Ujerumani, Sead Ramovi, amesimamishwa kwa muda na klabu ya CR Belouizdad baada ya mvutano mkali kati yake na uongozi wa klabu hiyo. Hatma yake sasa inasubiri uamuzi wa kamati ya nidhamu ya klabu utakaotolewa Jumanne ijayo.
Kulingana na mtandao wa Xtra90, Rais wa CR Belouizdad, Badreddine Bahloul alimwalika Ramovic kuhudhuria kikao cha dharura majira ya saa 4 usiku, huku akielekezwa kufika peke yake.
Ramovic, hata hivyo, alikataa wito huo akidai hakupokea taarifa yoyote rasmi, hakupokea barua, barua pepe wala mawasiliano mengine ya kiofisi. Aliomba kikao kifanyike kwa utaratibu rasmi na ndani ya saa za kazi.
Mvutano ulizidi pale Rais wa klabu alipotaka kuingilia chumba cha kubadilishia nguo wakati Ramovic akiwa katika kikao na wachezaji, akipitia mchezo uliopita na kuandaa mechi inayofuata.
Kocha huyo alisisitiza nidhamu na umakini wa timu, akiwataka viongozi kusubiri hadi kikao hicho kitakapomalizika kabla ya kuingilia shughuli za benchi la ufundi. Uongozi wa klabu uliripotiwa kutoridhishwa na msimamo huo.
Ramovic anafahamikwa kwa misimamo yake mikali kwani hata alipotua Yanga msimu uliopita aliacha kazi ghafla klabu ya TS Galaxy ya Afrika Kusini kwa kile alichoeleza kutofurahishwa na utaratibu wa klabu hiyo kuuza wachezaji muhimu kila msimu na kumvurugia mipango yake ya kushinda mataji.
Tangu ajiunge na CR Belouizdad, misimamo yake imemuingiza kwenye migogoro ya mara kwa mara na uongozi lakini kazi yake uwanjani imemfanya asalie na klabu hiyo kwa muda mrefu zaidi kinyume na matarajio ya wengi.
Licha ya kutofanya vizuri sana kwenye ligi ya ndani, Ramovic ameiongoza CR Belouizdad kufuzu nusu fainali ya michuano ya kombe la Shirikisho (CAFCC) msimu huu ikiwa ni mara ya kwanza kwa klabu hiyo kufikia mafanikio hayo.
Mashabiki wa Yanga bado wanamkumbuka Ramovic ambaye aliasisi soka la 'Gusa Achia Twende Kwao', wakitamani timu yao irejeshe aina hiyo ya soka.
Hivi karibuni Yanga ilimrejesha kocha msaidizi Abduhamid Moalin ambaye alifanya kazi na Ramovic akiwa kocha wake msaidizi.
Sasa kuna uwezekano mkubwa Ramovic akawa huru siku chache zijazo kwani kuna uwezekano mkataba wake utasitishwa CR Belouizdad.