Mshambuliaji wa Young Africans SC, Clement Mzize, ameendelea kuonyesha maendeleo mazuri ya kiafya na kuibua matumaini ya kurejea uwanjani mapema kabla ya msimu kumalizika.
Mzize, ambaye kwa sehemu kubwa ya msimu huu amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara, alifanyiwa upasuaji mwishoni mwa mwezi Februari nchini Afrika Kusini baada ya kuonekana kuwa na tatizo lililohitaji matibabu ya kina.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, mshambuliaji huyo alitarajiwa kukaa nje ya uwanja hadi mwishoni mwa msimu ili kukamilisha programu ya matibabu na mazoezi ya urejeaji.
Hata hivyo, taarifa mpya zinaeleza kuwa hali yake inaendelea kuimarika tofauti na matarajio ya awali, jambo ambalo limeongeza matumaini ndani ya kikosi cha Yanga.
Inaelezwa kuwa Mzize kwa sasa anaendelea kufanya mazoezi binafsi kwa juhudi kubwa, akilenga kuhakikisha anarejea haraka kuisaidia timu katika mechi za mwisho za msimu huu.
Mshambuliaji huyo ameonesha dhamira ya pekee ya kutaka kurejea mapema, akiongeza bidii katika mazoezi yake ya kila siku chini ya uangalizi wa karibu wa benchi la ufundi na timu ya kitabibu ya klabu.