Kiungo kiraka wa Yanga Duke Abuya jana aliondoka na tuzo ya nyota wa mchezo wa nusu fainali kombe la Muungano dhidi ya Azam Fc Wananchi wakitinga fainali baada ya ushindi wa mabao 2-1.
Kiungo huyo Mkenya aliondoka na tuzo hiyo baada ya kufanya kazi nzuri kwenye eneo la kiungo akishirikiana vyema na wenzake Mohamed Damaro 'Ngosha', Maxi Nzengeli na Allain Okello.
Msimu huu Duke amekuwa mchezaji muhimu sana katika kikosi cha Yanga, inawezekana jina lake halizungumzwi sana lakini hii ni silaha muhimu ya kocha Pedro Goncalves na benchi lake la ufundi.
Wakati Damaro akifanya kazi ya 'kukata umeme', Abuya alikuwa na jukumu la kusambaza 'pasi za upendo' akionekana kila eneo la uwanja bila ya kuchoka.
Duke na Maxi ni wachezaji ambao wanakimbia eneo kubwa la uwanja wakifanya kazi kubwa timu inapokuwa na mpira na hata bila ya mpira.
Duke amesema siri ya kung'ara kwake katika mchezo huo imetokana na kujituma pia ushirikiano aliopata kutoka kwa wachezaji wenzake.

