Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe ametamba kuwa watani zao Simba wameingia kwenye mtego baada ya hapo jana kufanikiwa kutinga fainali ya kombe la Muungano.
Yanga ilikuwa na kwanza kutinga fainali ya michuano hiyo juzi baada ya kuichapa Azam Fc mabao 2-1 na jana Simba kutinga hatua hiyo baada ya kuifunga Mlandege mabao 3-0.
Yanga na Simba zitachuana kwenye mchezo wa fainali utakaopigwa siku ya Jumatano, April 29 kabla ya timu hizo kurudiana tena May 03 katika mchezo wa ligi kuu ya NBC.
Kamwe amesema walitamani kukutana na Simba kabla ya mchezo wao wa ligi na hatimaye jambo hilo limetimia.
"Sisi tumefurahi kwa wao kuingia fainali kwani mitego yetu sasa imetimia," alitamba Kamwe.
Msimu huu Yanga na Simba tayari zimekutana mara mbili, mchezo wa kwanza ukiwa wa Ngao ya Jamii ambao Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kufuatiwa na mchezo wa ligi kuu uliopigwa dimba la New Amaan Complex na kumalizika kwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana.
Baada ya kupata sare hiyo, tambo zilikuwa nyingi upande wa Simba wakiamini walistahili kushinda wakitamba na matukio yaliyokuwa na faida upande wao.
Hata hivyo tangu March 1, Yanga imepitia mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na ujio wa kocha msaidizi Abdulhamid Moalin ambaye tangu aliporejesha Yanga imeshinda mechi zote huku ikifunga idadi kubwa ya mabao.
Kelele za Yanga kununua mechi zikaanza kusikika hadi kupelekea uongozi wa Yanga kuwachukua hatua baadhi ya wachambuzi waliokuwa wanasambaza propaganda hizo.
Ni wazi sasa mbele yake Yanga ina dakika 180 muhimu za kudhihirisha ufalme wao kwenye soka la Tanzania.