Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa fainali kombe la Muungano dhidi ya Simba ambao utapigwa kesho Jumatano, April 29 katika uwanja wa New Amaan Complex.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo, Goncalves amesema licha ya kuwa na vipaumbele vya mashindano, malengo ya timu ni kushinda kila mchezo unaokuja mbele yao.
Amesema wachezaji wake wamejiandaa sio kucheza fainali tu, pia kutoa burudani kwa mashabiki wao watakaojitokeza uwanja wa New Amaan Complex kushuhudia mchezo huo.
“Tulipoanza msimu tuliweka malengo yetu. Yapo mashindano ambayo yalikuwa kipaumbele chetu. Ukiachilia mbali kuwa na kipaumbele kwenye mashindano, msimamo wetu kama klabu ni lazima kushinda kila mechi bila kujali tupo mashindano gani. Kwa kuwa tupo hapa hatuna budi kushinda mchezo wowote uliopo mbele yetu”
“Mara nyingi huwa natazama zaidi mwenendo wa klabu yangu na si vinginevyo. Ninao wajibu wa kusaidia wachezaji wangu kuimarisha viwango vyao. Wachezaji wangu wote wapo vizuri. Wamejiandaa sio tu kucheza fainali bali kutoa burudani. Tutakwenda kuburudisha na sio tu kucheza fainali. Nina matarajio makubwa kutoka kwa vijana wangu”
“Yanga inapokuwa ndani ya Tanzania Bara au visiwani ipo nyumbani. Yanga inapokwenda popote ndani ya Tanzania ipo nyumbani. Tumepata mapokezi mazuri sana kila sehemu tuliyokwenda. Hapa Zanzibar tupo nyumbani. Natarajia kuona mashabiki wakimiminika kwa wingi uwanjani siku ya fainali. Natamani kushangilia pamoja na mashabiki hapo kesho,” alisema Pedro