Licha ya kupoteza mchezo dhidi ya Dodoma Jiji jana, Yanga bado iko kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na alama zake 54.
Gap dhidi ya Simba inayoshika nafasi ya pili ni alama 2 huku zikiwa zimesalia mechi 7 kuhitimisha msimu.
Katika mechi zilizobaki, Yanga itasafiri nje ya jiji la Dar es salaam kwenye mechi mbili dhidi ya Mashujaa Fc na Fountain Gate na mechi tano ziiizobaki zote zitapigwa jijini Dar es salaam.
Mechi zilizobaki Dar ni dhidi ya Singida BS, Namungo Fc, TRA United, Azam Fc na JKT Tanzania.
Mechi nne za nyumbani zitapigwa dimba la KMC Complex wakati mchezo dhidi ya JKT Tanzania ukipigwa uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Yanga itakwenda Mbweni mara mbili kuikabili JKT Tanzania kwani Jumamosi timu hizo zitakutana kwanza kwenye mchezo wa robo fainali kombe la CRDB.
Yanga ina faida zaidi dhidi ya Simba endapo itatokea zikalingana pointi kwani kigezo cha kwanza kinachoangaliwa kwenye msimamo ni matokeo ya jumla baina ya timu zilizolingana (H2H).
Yanga ilifunga mabao mawili ugenini dhidi ya Simba katika mchezo wa mkondo wa pili huku mchezo wa mkondo wa kwanza ukimalizika kwa suluhu ya bila kufungana.
Kama msimu uliopita Wananchi walilinda gap la pointi moja hadi ubingwa, mafanikio hayo yanaweza kurudiwa tena msimu huu.
Kwa kugha rahisi ni kuwa ubingwa bado uko mikononi mwa Yanga, ili timu nyingine ziweze kutwaa ubingwa, ni lazima Yanga ifanye makosa.
Kazi iliyo mbele ya wachezaji na benchi la ufundi ni kuhakikisha makosa hayo hayajitokezi katika mechi 7 zilizobaki.