Yanga Princess leo imekubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Simba Queens matokeo ambayo yamefifisha matumaini kwa Yanga Princess kwenye mbio za ubingwa wa ligi kuu ya Wanawake.
Yanga Princess iliuanza taratibu mchezo huo uliopigwa uwanja wa Azam Complex na kuwapa nafasi Simba Queens kutawala na kupata mabao mawili mapema kwenye kipindi cha kwanza kupitia kwa Jentrix Shikangwa.
Princess walirejea kipindi cha pili wakiwa imara zaidi wakipata bao la kwanza kupitia kwa Riticcia Nabossa kwenye dakika ya 58. Bao hilo lilitokana na mpira wa faulo uliopigwa na Precious Christopher baada Jeaninne Mukandayisenga kufanyiwa madhambi katika tukio ambalo lilionekana kama ndani ya eneo la hatari na pengine mwamuzi alistahili kutoa mkwaju wa penati na adhabu kwa mchezaji wa Simba Queens lakini hakufanya hivyo.
Licha ya kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa Simba Queens kwenye kipindi cha pili, jitihada za kikosi cha kocha Edna Lema hazikuzaa matunda na kujikuta wakikubali kipigo hicho.
Yanga Princess imebaki nafasi ya pili ikiwa na alama 39 huku Simba Queens wakiongoza ligi na alama 46.