Inaelezwa Yanga imepiga hatua kubwa katika jitihada za kumrejesha aliyekuwa kiungo wake mshambuliaji Stephan Aziz Ki ambaye kwa sasa anaitumikia Al Ittihad ya Libya aliyojiunga nayo akitoka klabu Wydad CA ya Morocco.
Msimu uliopita Yanga ilimuuza Aziz Ki kwenda Wydad hata hivyo Ki aliitumikia Wydad kwa miezi sita tu na baadae kuelekea Libya akitua Al Itihad kwenye usajili wa dirisha dogo mwezi Januar 2026.
Habari kutoka chanzo cha uhakika ni kuwa Aziz Ki yuko tayari kurejea Yanga hasa kutokana na changamoto za kiusalama alizokumbana nazo huko Libya.
Lakini pia nyota huyo kutoka Burkina Faso anataka kurejea nchini ili aungane na familia yake ambapo mkewe Hamisa Mobeto yuko nchini.
“Aziz KI anataka kurudi Yanga, kuna mambo yanaendelea chinichini, bado ana mkataba na timu yake kwa kuwa Januari ndiyo alijiunga nayo na kusaini miaka miwili."
“Tunaweza kuwa na timu imara msimu ujao, kuna wachezaji wazuri wanataka kuja hapa kwetu. Aziz KI hafurahii maisha ya kule Libya, tunalifikiria hili pia,” chanzo kilinukuliwa na Mwanaspoti
Ikumbukwe kuwa, Februari 16, 2025, Aziz Ki alifunga ndoa na mwanamitindo Mobeto jijini Dar es Salaam, lakini staa huyo amekuwa akifanya biashara zake hapa jijini Dar es Salaam na amekuwa akienda Libya mara chache kuungana na mume wake.
“Ukiacha hilo kuna suala la familia yake, unakumbuka Aziz ameoa hapa, amekuwa mbali na familia yake, hili linamtesa, anaona ni bora arejee hapa kuwa karibu na mke wake.”
Aziz Ki aliitumikia Yanga kwa misimu mitatu akiweka rekodi ya kupachika mabao zaidi ya 50 huku akiondoka na tuzo za MVP na mfungaji bora wa ligi kuu