Kocha Mkuu wa Yanga Abdihamid Moalin amesema hana mashaka na uwezo wa nahodha wa timu hiyo Bakari Nondo Mwamnyeto na ataendelea kumuunga mkono kwa sababu anajua umuhimu wake kikosini.
Moalin ametoa kauli hiyo kufuatia kile kilichotokea mkoani Singida kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Dodoma Jiji ambapo Mwamnyeto alijifunga katika jitihada za kuokoa hatari langoni tukio ambalo lilimletea mashambulizi mengi mitandaoni.
Moalin amesema makosa ni sehemu ya maisha ya Mwanadamu na yuke anayeogopa kufanya makosa hawezi kuonyesha ubora wala kujiamini akiwa uwanjani.
“Kila mtu anamjua Bakari Mwamnyeto ni mchezaji mkubwa na mwenye heshima kubwa, sio tu ndani ya Yanga bali pia kwenye soka la Tanzania kwa ujumla."
"Siwezi kujaadili uwezo wake kwa sababu ni jambo ambalo lipo wazi kwa kila mtu anayefuatilia mpira. Makosa ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, sio kwenye mpira pekee. Kama unaogopa kufanya makosa basi huwezi kuonesha ubora wako wala kujiamini ukiwa uwanjani."
"Wachezaji wakubwa duniani pia hufanya makosa, lakini kinachowatofautisha ni namna wanavyorudi na kupambana zaidi. Bakari ni kiongozi ndani na nje ya uwanja. Ana uzoefu mkubwa, anaipambania timu kila wakati na mchango wake kwa Yanga ni mkubwa sana."
"Tuna imani kubwa naye na tunaendelea kumuunga mkono kwa sababu tunajua uwezo alionao na kile anachoweza kuifanya timu hii,” alisema Moalin