Kiungo mshambuliaji wa Al Ittihad Stephane Aziz Ki amedokeza uwezekano wake wa kurejea kwa waajiri wake wa zamani klabu ya Yanga msimu ujao.
Katika video inayosambaa mitandaoni ikimuonyesha Aziz Ki akiwa na msanii wa bongofleva Ommy Dimpoz walipokutana nchini Ufaransa, Ki ameweka wazi baada ya kuulizwa na Dimpoz tetesi zinazomuhusisha kurejea kwa Wananchi.
Ommy Dimpoz alionekana kumuuliza moja kwa moja kuhusu tetesi hizo akisema:
“Nimesikia unarejea Yanga,” aliuliza Dimpoz huku Aziz Ki nae akijibu kwa ufupi; “Insha’Allah! Huwezi jua, Insha’Allah.”

Inaelezwa tayari uongozi wa Yanga umeanza mchakato wa kukamilisha usajili wake baada ya Aziz Ki mwenyewe kuweka wazi hitajio lake la kurejea Tanzania kuungana na familia yake.
Aziz Ki alijiunga na Al Ittihad mapema mwaka huu kwenye usajili wa dirisha dogo akitokea klabu ya Wydad CA ya Morocco.
Hata hivyo changamoto za usalama huko Libya na dhamira ya kuungana na familia, vimechangia kiungo huyo wa Kimataifa wa Burkina Faso kutaka kurejea Tanzania.