Kikosi cha Yanga kinaendelea na maandalizi yake kuelekea mechi muhimu za kuhitimisha msimu ligi kuu ya NBC na kombe la CRDB.
Yanga ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo na mkakati ni kuhakikisha mataji hayo yanasalia Jangwani kwa msimu wa tano mfululizo.
Ni wiki ya mchaka-nmchaka kwa kuwa kuanzia Jumamosi, Juni 13 hakutakuwa na muda tena wa kujiandaa kutokana na ukaribu wa mechi.
Katika muda wa siku 17 kuanzia Juni 13 Yanga itacheza mechi 6 ukiwa ni wastani wa kucheza kila baada ya siku tatu.
Makocha wa Yanga Abdilhamid Moalin na Patrick Mabedi watatumia wiki hii kukamilisha maandalizi muhimu iili kuhakikisha wachezaji wanakuwa tayari kwa ratiba hiyo ngumu inayokuja mbele yao.
Hakuna nafasi ya kufanya makosa tena, kwani matokeo tofauti na ushindi kwenye kila mchezo yatawanufaisha wapinzani wao Simba kwenye mbio za ubingwa wa ligi kuu.
Yanga itakuwa salama kutetea ubingwa wake kama itakusanya angalau alama 13 kutoka mechi 5 zilizobaki huku ikikabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Azam Fc ambao watacheza nao mara mbili, TRA United na JKT Tanzania.
Kikosi cha Yanga kitaanzia ratiba yake mkoani Kigoma siku ya Jumamosi kwa mchezo dhidi ya Mashujaa Fc utakaopigwa uwanja wa Lake Tanganyika.