Uongozi wa Yanga unafanya kwa usiri mkubwa mchakato wa kusaka kocha mpya baada ya kumfuta kazi Pedro Goncalves mwezi uliopita.
Malengo ya Yanga ni kuhakikisha wanampata kocha mpya kabla ya msimu huu kumalizika ili apate muda wa kukifuatilia kikosi na kuweka mapendekezo yake kwa aina ya maboresho anayohitaji.
Yanga haitaki kurudia makosa ya msimu uliopita ambapo baada ya kuachana na Miloud Hamdi walichukua muda mrefu kumpata kocha Romain Folz ambaye hata hivyo hakuweza kumudu presha ya kuwanoa mabingwa hao wa nchi akifutwa kazi baada ya kuiongoza Yanga kwenye mechi mbili tu za ligi.
Mpaka sasa kuna tetesi nyingi kuhusu kocha ajae Yanga lakini ukweli ni kuwa mchakato huo unafanywa kwa usiri mkubwa. Lakini jambo la uhakika ni kuwa wakati huu Yanga haitafanya 'bahati nasibu' kumpata kocha.
Miongoni mwa vigezo vilivyowekwa kocha huyo ni lazima awe na uzoefu mkubwa wa soka la Afrika na zaidi awe amepata mafanikio kwenye mashindano ya CAF kwa timu alizozinoa.
Kocha wa zamani wa Yanga Nasreddine Nabi ni miongoni mwa majina yanayotajwa lakini pia tetesi zikimtaja kocha wa zamani wa Al Ahly na Mamelodi Sundowns, Pitso Mosimane.
Mosimane amekuwa na urafiki wa karibu na Rais wa Yanga Ijinia Hersi Said ambapo mwishoni mwa mwaka jana alitua nchini kuzindua Yanga Soccer School mradi wa Shule ya soka ya Yanga.
Mosimane pia aliwahi kuja nchini akawa mgeni rasmi kwenye Wiki ya Mwananchi katika tukio ambalo lilimshangaza na tangu wakati huo amekuwa karibu na uongozi wa Yanga.
Mosimane alijipa likizo ya masuala ya ukufunzi wa klabu akijikita zaidi kwenye kuibua vipaji. Hata hivyo inaelezwa yuko tayari kurejea katika majukumu makubwa ya klabu.
Katika orodha hiyo pia yumo kocha wa zamani wa Yanga Miguel Gamondi ambaye kwa sasa ni kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' ambapo kwa majukumu yake ya sasa huenda ikawa ngumu kwa Yanga kumpata.
Lakini pia yapo majina ya Miloud Hamdi aliyeipa Yanga ubingwa wa ligi kuu na kombe la CRDB msimu uliopita na makocha wa zamani wa Simba steve vandebroek na Fadlu Davids.
Jina la mkufunzi wa Asec Mimosas Julien Chevalier pia ni miongoni mwa majina yanayotajwa kuwa kwenye orodha ya makocha wanaohitajika Jangwani. Yanga ilijaribu kumpata Chevalier bila mafanikio msimu uliopita kabla ya ujio wa Folz
Lakini pia makocha wa sasa Abdilhamid Moalin na Patrick Mabedi wanaweza kuachiwa majukumu kikamilifu kama wataiwezesha Yanga kufanikisha malengo ambayo ni kutetea mataji ya ligi kuu na kombe la CRDB.
Yanga inatarajiwa kumtangaza kocha mpya baada ya msimu kumalizika ambapo ataanza majukumu yake na kikosi wakati wa pre-season