Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema kwa sasa kipaumbele cha timu hiyo ni kuhakikisha wanatetea mataji mawili yaliyosalia yaani ligi kuu na kombe la CRDB.
Licha ya kuhusishwa na tetesi mbalimbali za usajili, Kamwe amesema kwa sasa viongozi wameweka nguvu zaidi kwenye kutimiza malengo ya timu na hivyo hakuna michakato yoyote usajili inayofanyika.
"Kwa sasa hakuna mazungumzo yoyote mbayo tunafanya iwe kocha au wachezaji kwa sababu tuna jukumu kubwa mbele yetu"
"Malengo ya uongozi wa Yanga ni kuiandaa timu kuelekea mechi tano za Ligi Kuu zilizobakia pamoja na mchezo wa nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB"
"Mazungumzo yaliyoanza kwa sasa ni kwa ajili ya kuongeza mikataba baadhi ya wachezaji inayomalizika mwisho wa msimu huu."
"Tunawaomba Wanachama na Mashabiki wetu kuweka nguvu kubwa kwenye mechi hizo kwa kuja kwa wingi viwanjani na kuwaombea dua wachezaji wetu ili waweze kuipambania kwa Jasho lao lote heshima ya Yanga na kuweza kutwaa makombe mawili yaliobaki," alisema Kamwe
Yanga inaendelea na maandalizi yake kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mashujaa Fc ambao utapigwa Jumamosi, Juni 13 katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.