Mshambuliaji Laurindo Aurelio 'Depu' jana aliingia dakika ya 86 kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mashujaa Fc lakini dakika chache alizotumika zilitosha kuwapa ujumbe benchi la ufundi la Yanga kuwa anahitaji dakika zaidi za kucheza.
Akitoka kwenye majukumu ya timu ya Taifa ya Angola, pengine hakupewa dakika nyingi kutokana na uchovu kwani alirejea siku moja kabla ya mchezo huo.
Depu alimanusra aifungie Yanga bao kama sio umahiri wa mlinda lango wa Mashujaa Fc aliyeokoa shuti lake lililokuwa linaelekea kimiani.
Hata hivyo ni yeye aliyetoa pasi ya bao kwa nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto aliyepigilia msumari wa pili na kuihakikishia Yanga ushindi muhimu mkoani Kigoma.
Pengine Depu anaweza kuwa amejihakikishia nafasi ya kuanza kwenye mchezo ujao dhidi ya Fountan Gate utakaopigwa Jumatano uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha kutokana na kile alichofanya kwa dakika chache kwenye mchezo dhidi ya Mashujaa Fc.
Mshambuliaji namba moja Prince Dube bado anaendelea kukabiliana na ukame wa mabao akiwa amesimama kwa muda mrefu kwenye mabao 9.