Kocha Mkuu wa Yanga Abdihamid Moalin amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya TRA United ambao utapigwa kesho Jumamosi kwenye uwanja wa KMC Complex.
Moalin amesema amekiandaa kikosi kimbinu kukabiliana na TRA United huku akitarajia upinzani mkali kutoka kwa wakusanya ushuru hao.
"TRA United ni timu nzuri yenye wachezaji wazuri. Wanapenda kushambulia kwa kutumia mawinga wao na kupiga krosi kwa wingi. Tunajua nini tunapaswa kufanya katika kukabiliana nao"
"Lakini pia nasi tumejiandaa vyema na kuhakikisha tunashinda mchezo huo. Nina imani kubwa kwa wachezaji wangu, tutakwenda kutimiza vyema mpango wetu wa mechi na kuweza kushinda"
"Tunawaheshimu TRA United na tunajua utakuwa mchezo mgumu lakini hakuna kitakachobadilika kwenye malengo yetu, tunahitaji ushindi."
"Nimewaambia wachezaji wangu hatupaswi kuwa na presha, tutacheza kwa kuzingatia mpango wetu wa mchezo huku tukiwaheshimu wapinzani wetu"
"Ninafurahi kuongoza kikosi hiki chenye wachezaji bora ambao wako tayari kupambana kila mara kwa kuzingatia mahitaji ya mchezo husika," alisema Moalin