Kocha Mkuu wa Yanga Abdihamid Moalin amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa kukamilisha msimu wa ligi kuu dhidi ya JKT Tanzania ambao utapigwa kesho Jumanne kwenye uwanja wa Isamuhyo.
Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo, Moalin amesema malengo ya Yanga ni kushinda mchezo huo na kuhakikisha wanatetea taji la ligi kuu.
Moalin amesema wanatarajia kukutana na upinzani mkali dhidi ya JKT Tanzania, miongoni mwa timu bora kwenye ligi msimu huu.
"Utakuwa mchezo mgumu, JKT Tanzania ni moja ya timu ngumu, inafundishwa na moja ya makocha bora kwenye ligi kuu ya NBC msimu huu."
"Tulicheza nao hapa mara ya mwisho kwenye mchezo wa robo fainali kombe la CRDB, hivyo tunafahamu upinzani ugumu tunaokwenda kukutana nao, tutahitaji kuwa kwenye ubora wetu kama tulivyofanya mchezo uliopita."
"Sisi tunakwenda kucheza kwa kuzingatia malengo tuliyojiwekea, tunahitaji kushinda. Sisi sio timu kukaa nyuma kuzuia, tunahitaji kucheza mpira na kufunga magoli."
"Yanga ni timu kubwa tuna wachezaji wazuri wanaoweza kutupa matokeo tunayohitaji hivyo kesho tutakwenda uwanjani tukiwa na lengo la kushinda," alisema Moalin.
Mchezo huo hutakaopigwa saa 10 jioni, unaweza kuishuhudia Yanga ikitetea taji la ligi kuu endapo wataibuka na ushindi au hata matokeo ya sare yanaweza kuwatosha Wananchi kurejesha taji hilo Jangwani na kuendeleza rekodi ya kibabe kwenye ligi kuu ya Tanzania Bara