Mshambuliaji wa Yanga Emmanuel Mwanengo amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo hapo kesho kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya JKT Tanzania.
Mchezo huo wa kuhitimisha msimu utapigwa saa 10 jioni Yanga ikihitaji ushindi ili kutwaa ubingwa.
Licha ya ubora wa JKT Tanzania, Mwanengo amesema wao wanahitaji ushindi wa aina yoyote kuweza kuwa mabingwa hivyo wachezaji watakwenda kupambana ili kuhakikisha wanafanikisha mpango wa ushindi lakini itakuwa rahisi zaidi kama Wananchi watafurika dimba la Isamuhyo.
“JKT Tanzania ni timu nzuri na walitupa mechi ngumu kwenye kombe la CRDB. Naamini kimbinu watakuwa wamejiandaa vizuri pia, lakini sisi ni Yanga, tunapaswa kuwa bora zaidi ili kushinda mchezo wa kesho”
“Uzuri wa mchezo wa kesho hauhitaji ushindi mkubwa, unahitaji alama tatu tu, hata tukishinda goli moja tutatangazwa kuwa mabingwa, hivyo niwaombe Wananchi waje kwa wingi kwasababu uwepo wao ni nguvu kubwa kwetu, waje tushinde pamoja,” alisema Mwanengo.
Alama tatu zitatosha Yanga kuwa mabingwa licha ya kuwa wanaweza kutetea ubingwa pia wakipata matokeo ya sare.
Kama Yanga itatoka sare, Simba itahitaji kupata ushindi wa angalau mabao 17-0 kuweza kuwa mabingwa.