Mlinzi wa kushoto wa Yanga Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' jana alitwaa taji lake la kwanza la ligi kuu tangu alipojiunga na mabingwa hao wa kihistoria Tanzania Bara.
Lilikuwa taji la tano mfululizo kwa Yanga baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania pia likiwa taji la 32 kihistoria kwa Yanga.
Zimbwe Jr alikuwa sehemu ya kikosi kilichohakikisha ubingwa huo wa kihistoria kwa klabu ya Yanga.
Hata hivyo unaweza kusema ni ubingwa ambao ulimfanya Zimbwe Jr ashangilie kwa hisia sana kutokana na kile alichopitia tangu ajiunge na Yanga akitokea klabu ya Simba msimu uliopita.

Zimbwe Jr aliitumikia Simba kwa takribani miaka 10 kabla ya kutua Yanga, uhamisho ambao ulimletea changamoto nyingi za nje ya uwanja.
Meneja wa mchezaji huyo Carlos Sylvester a,k.a Carlos Mastermind nae alibubujikwa na machozi ya furaha jana baada ya Yanga kutwaa ubingwa huku akiweka wazi changamoto ambazo yeye na mteja wake wamepitia baada ya kuondoka Simba.
Mastermind ameweka wazi kuwa mteja wake alipitia kipindi kigumu sana ambapo beki huyo alikumbana na mateso ya kisaikolojia, kukosolewa vikali, kutukanwa, na hata kutishiwa maisha na mashabiki kutokana na uamuzi wake wa kuhama klabu.
Meneja huyo alieleza kwa hisia kuwa Zimbwe Jr alikuwa akilia kila walipokutana kutokana na maumivu ya maneno hayo hasa ikizingatiwa alijitoa kuitumikia timu hiyo tena akiwa nahodha kwa misimu kadhaa.
Ama kwa hakika ilikuwa siku ya kipekee kwake, kwani amewafunga midomo wale wote waliokuwa wakimuombea mabaya na kuona hafanikiwa akiwa na Yanga.
Ametwaa taji la tatu Yanga akiwa pia sehemu ya kikosi kilichotwaa Ngao ya Jamii na kombe la Mapinduzi