Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, wanatajwa kuwa katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa winga chipukizi wa Fountain Gate FC, Juma Abushiri maarufu kama Chuga Boy, katika kile kinachoonekana kuwa moja ya dili zinazovuta hisia kwenye dirisha hili la usajili.
Kwa mujibu wa taarifa, Chuga Boy alikuwa tayari amepata nafasi ya kuelekea klabu ya Gent ya Ubelgiji kwa ajili ya majaribio, huku ikielezwa kuwa safari yake ilitarajiwa kuanza Agosti 12, 2026.
Hata hivyo, Yanga imeingia kati katika hatua za mwisho kwa kumuwekea mezani ofa ya kuvutia, ikiwemo mkataba wa miaka mitatu, makubaliano binafsi na mchezaji yakiwa tayari yamefikiwa. Yanga italazimika kukubaliana na Fountain Gate kuhusu ada ya uhamisho wa mchezaji huyo.
Chuga Boy amekuwa mmoja wa vipaji vinavyochipukia kwa kasi kwenye soka la Tanzania kutokana na uwezo wake wa kucheza pembeni, kasi, ubunifu na uthubutu wa kuwavaa mabeki.
Usajili wa winga huyo ni sehemu ya mkakati wa Yanga kuendelea kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu wa 2026/27, ambapo pamoja na kutetea mataji ya ndani, klabu hiyo inalenga kufanya vizuri zaidi kwenye michuano ya kimataifa.
Yanga imepania kuongeza nguvu eneo la washambuliaji wa pembeni baada ya kukabiliwa na changamoto kwenye maeneo hayo msimu uliomalizika