Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, wametajwa kuwa katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa beki wa kushoto wa Mouna FC ya Ivory Coast, Samba Koné.
Yanga inamsajili Koné mwenye umri wa miaka 23 kama mbadala wa beki kutoka DR Congo, Chadrack Boka, ambaye mkataba wake umemalizika
Koné, ambaye ni raia wa Ivory Coast, amejijengea sifa kubwa msimu uliopita kutokana na kiwango chake bora akiwa upande wa kushoto wa ulinzi wa Mouna FC.
Beki huyo ametajwa kuwa mmoja wa mabeki bora wa kushoto katika Ligi Kuu ya Ivory Coast baada ya kutoa pasi nne za mabao na kuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya timu yake.
Mbali na mafanikio hayo, Koné pia ana uzoefu wa kucheza nje ya nchi yake baada ya kuwahi kuitumikia Paradou AC ya Algeria, klabu inayojulikana kwa kukuza vipaji vya soka barani Afrika.
Uzoefu huo unaelezwa kuwa moja ya sababu zinazowavutia viongozi wa Yanga ambao wanataka kuongeza ushindani kwenye kikosi chao kuelekea michuano ya kimataifa msimu ujao.
Mkataba wa Koné na Mouna FC ulifika tamati Juni 30 mwaka huu hivyo anatarajiwa kujiunga na Yanga akiwa mchezaji huru.
Yanga inaendelea na mkakati wa kuimarisha kikosi chake baada ya msimu wenye ushindani mkali Wananchi wakifanikiwa kutetea taji la ligi kuu kwa msimu wa tano mfululizo.