Winga wa Al Hilal ya Sudan, Jean Giramugisha, ametwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Rwanda (MVP) kwa msimu wa 2025/26 baada ya kutangazwa mshindi katika hafla ya utoaji wa tuzo iliyofanyika usiku wa Jumapili.
Giramugisha ameshinda tuzo hiyo kutokana na kiwango chake bora alichokionyesha msimu mzima, akijitambulisha kama mmoja wa wachezaji waliokuwa na ushawishi mkubwa zaidi katika Ligi Kuu ya Rwanda.
Kasi yake, ubunifu na uwezo wa kucheza katika nafasi mbalimbali za ushambuliaji vimemfanya kuwa mmoja wa nyota waliovutia macho ya wengi ndani na nje ya Afrika.
Baada ya msimu wake wa kuvutia, klabu kadhaa zimeonyesha nia ya kumsajili. Mabingwa wa Tanzania, Yanga SC, wanatajwa kuwa miongoni mwa klabu zinazoongoza katika mbio za kuwania saini yake, huku pia akihusishwa na klabu mbalimbali za kimataifa. Miongoni mwa klabu zinazoripotiwa kumfuatilia ni Sporting Lisbon ya Ureno.
Klabu nyingine zinazotajwa kumuhitaki winga huyo hatari ni AS Saint-Etienne ya Ufaransa Pyramid Fc ya Misri, Far Rabat ya Morocco, Al Ahli Tripoli ya Libya na Ahly Benghazi ya Libya
Ni wazi kutwaa tuzo ya MVP kumeongeza thamani ya Giramugisha kwenye soko la usajili, na huenda vita ya kuwania saini yake ikawa miongoni mwa simulizi kubwa za dirisha hili la usajili.
Pamoja na usajili huu kuonekana kama 'HAIWEZEKANI' kwa Yanga, inaelezwa mkakati wa mabingwa hao wa soka nchini kwenye dirisha hili ni kusajili wachezaji wenye profile kubwa wakiweka malengo ya kufanya vyema zaidi kwenye michuano ya ligi ya mabingwa.
"Kuna sajili ambazo wengi wanaona kama haiwezekani zitafanyika! Wewe subiri tu mambo yakamilike kuna watu hawataamini kile tunachokwenda kufanya kwenye dirisha hili," alizungumza kwa kujiamini mmoja wa viongozi waandamizi Yanga.