Klabu ya AS FAR imeingia katika mbio za kumuwania winga wa Kaizer Chiefs Glody Makabi Lilepo, imefahamika.
AS FAR inayonolewa na aliyekuwa kocha wa Yanga Pedro Goncalves aliyejiunga na timu hiyo hivi karibuni, inatajwa kuweka mezani ofa ya dola milioni 1 (zaidi ya Tsh 2.6B) kumnasa winga huyo ambaye ameutaarifu uongozi wa Kaizer Chiefs anataka kuondoka.
Lilepo hayupo kwenye kikosi cha Chiefs kilichoanza pre-season akipewa ruhusa ya kushughulikia uhamisho wake. Mcongomani huyo bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Chiefs.
Inaelezwa Kocha Mkuu wa Yanga Manqoba Mngqithi alihitaji huduma ya winga huyo ambaye msimu uliopita aliifungia Chiefs mabao matano na kutoa pasi nne za mabao.
Ushindani unaonekana kuwa mkali kuipata saini yake na pengine huenda Yanga ikatupia macho kwa nyota wengine kwa kuzingatia mahitaji yake.

Manqoba anamtaka winga mwingine Stellenbosch
Kulingana na mtandao wa FARPost wa Afrika Kusini, Yanga imeulizia upatikanaji wa winga hatari wa Stellenbosch, Langelihle Phili (21)
Stellenbosch wameweka wazi kuwa timu inayomuhitaji nyota huyo inapaswa kulipa gharama ya kuvunja mkataba wake takribani dola milioni 1.
Nyota huyo pia anawaniwa na klabu ya Kaizer Chiefs huku msimamo wa Stellenbosch ukiwa ni kufanya biashara na timu ambayo itakuwa tayari kulipa 'buyout close'.
Inaelezwa Mngqithi amependekeza maboresho kwenye maeneo muhimu ambayo amehitaji yafanyike baada ya kufanya tathmini.
Manqoba anayetarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa wiki hii, anafanya kazi kwa karibu na Kamati maalum iliyopewa jukumu la kusimamia michakato ya usajili.