Kocha Mkuu wa Yanga Manqoba Mngqithi tayari yuko nchini kuanza majukumu yake ya kuwanoa mabingwa hao wa soka Tanzania Bara.
Inaelezwa Manqoba ametua nchini akiongozana na 'Performance Analyst', Yardaan Valodia, makocha wasaidizi Simo Dladla na Kagisho Dikgacoi wote raia wa Afrika Kusini. Pia yumo kocha wa magolikipa Greg Etafia
Yanga itangia rasmi kambini Jumatatu, Julai 20 kuanza maandalizi kuelekea msimu mpya wa mashindano 2026/27.
Manqoba na benchi lake la ufundi watakuwa na takribani wiki tatu za kukiandaa kikosi kabla ya mchezo wa kwanza wa mashindano dhidi ya Simba, mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa Agosti 12.
Mchezo huu utakuwa kipimo cha kwanza kwa Manqoba dhidi ya kocha mwenzake kutoka Afrika Kusini Steve Barker anayeinoa Simba.
Lakini pia mchezo huu unaweza kutoa taswira ya kile mashabiki wa Yanga watarajie msimu wa 2026/27.
Uongozi wa Yanga umeweka malengo makubwa msimu ujao kwani licha ya kuhitaji kutwaa mataji yote ya ndani, mabingwa hao wa kihistoria wanakiu ya kufanya vyema zaidi kwenye michuano ya ligi ya mabingwa ambapo mechi za mtoano hatua ya awali zinatarajiwa kupigwa mwanzoni mwa Septemba 2026.