Kocha mpya wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu sababu zilizomshawishi kujiunga na mabingwa hao wa Tanzania, akieleza kuwa ilikuwa ni fursa ambayo hakuweza kuipuuza.
Mngqithi ametua Yanga baada ya kuachana na Golden Arrows mwishoni mwa msimu wa 2025/26, ambapo aliiongoza timu hiyo kumaliza katika nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini (Betway Premiership).
Kocha huyo amesema Yanga imekuwa ikihitaji huduma yake kwa muda mrefu, lakini sasa ndipo alipoona wakati mwafaka wa kukubali changamoto hiyo mpya.
"Kwangu mimi, hii ni fursa ambayo kila kocha angependa kuikumbatia kwa mikono miwili na kuona inaweza kumfikisha wapi. Nimefurahi sana kuwa hapa," alisema Mngqithi.
Aliongeza kuwa mazungumzo kati yake na Yanga yalianza kitambo, lakini safari hii mazingira yalikuwa rafiki zaidi kwa kuwa hakuwa chini ya mkataba na klabu nyingine.
"Wamekuwa wakinisaka kwa muda mrefu. Safari hii ilikuwa rahisi kwa sababu sikuwa nimefungwa na klabu yoyote. Nikaona ni wakati sahihi wa kujaribu changamoto hii."
Kwa mujibu wa Mngqithi, moja ya sababu kubwa zilizomvutia kujiunga na Yanga ni ubora wa klabu hiyo, ambayo anaamini ina kila kitu kinachohitajika kushindania mataji makubwa ndani na nje ya Tanzania.
"Yanga ni klabu yenye kila kitu kinachohitajika kushindana katika kiwango cha juu. Lakini kilichonivutia zaidi ni watu waliopo ndani ya klabu. Nilikutana na watu wenye utu mkubwa, jambo lililonifanya nikubali kuja hapa."
Kariakoo Derby yamvutia
Mbali na kuzungumzia ujio wake Yanga, Mngqithi pia alieleza kufurahishwa na uwezekano wa kukutana na kocha mwenzake kutoka Afrika Kusini, Steve Barker, ambaye kwa sasa anaiongoza Simba SC.
Mchezo wa Kariakoo Derby unatarajiwa kuwa moja ya mechi zitakazovuta hisia kubwa, huku makocha hao wawili kutoka taifa moja wakitarajiwa kuonyeshana uwezo wao kwa mara ya kwanza katika soka la Tanzania.
"Ni jambo la kusisimua sana. Ninaelewa kwa nini mashabiki wengi wanasubiri kwa hamu kuona makocha wawili kutoka Afrika Kusini wakikutana kwenye Kariakoo Derby," alisema Mngqithi.
Ujio wa Manqoba Mngqithi unaashiria mwanzo wa enzi mpya ndani ya Yanga, huku mashabiki wakitarajia kuona timu ikiendelea kutawala soka la Tanzania na kufanya vizuri zaidi katika michuano ya kimataifa.
Kocha huyo anaingia akiwa na uzoefu mkubwa wa soka la Afrika, jambo linaloongeza matumaini kwamba ataweza kuipeleka Yanga katika mafanikio mapya ndani ya msimu ujao.