Nahodha wa Yanga SC, Bakari Mwamnyeto, ataendelea kusalia ndani ya kikosi cha Wananchi baada ya kufikia makubaliano ya kuongeza mkataba wake na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Taarifa zinaeleza kuwa baada ya majadiliano yaliyodumu kwa wiki kadhaa, pande zote mbili zimefanikiwa kufikia mwafaka, hatua inayomaliza uvumi kuhusu mustakabali wa beki huyo ndani ya klabu.
Mwamnyeto ni mmoja wa wachezaji wenye uzoefu mkubwa katika kikosi cha Yanga, akiitumikia klabu hiyo kwa takribani misimu sita. Katika kipindi hicho, ameonyesha uongozi mkubwa uwanjani na kuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya timu.
Chini ya uongozi wake, Yanga imefanikiwa kutwaa mataji matano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, pamoja na mataji mengine ya Kombe la FA, Ngao ya Jamii na mashindano mengine ya ndani.
Kuongezwa kwa mkataba wa Mwamnyeto ni sehemu ya mkakati wa Yanga wa kuendelea kuhifadhi wachezaji wake muhimu kuelekea msimu mpya, huku klabu ikilenga kuendeleza mafanikio yake katika mashindano ya ndani na kimataifa.