Yanga SC imefanikiwa kupata moja ya vipaji vikubwa vinavyochipukia kwenye soka la Tanzania baada ya kumsajili Juma Issa Abushiri, maarufu kama Chuga Boy.
Mzaliwa wa Mei 20, 2008, kutoka mkoani Arusha, Abushiri ni kiungo mshambuliaji anayependa pia kucheza winga wa kulia. Licha ya umri wake mdogo, tayari ameonyesha uwezo mkubwa unaowafanya wengi kumuona kama nyota wa baadaye wa soka la Tanzania.
Chuga Boy anajulikana kwa uwezo wake mkubwa wa kukimbia na mpira, kuwatoka mabeki kwa chenga, pamoja na kutengeneza nafasi. Mtindo wake wa uchezaji umewafanya mashabiki wengi kumpa jina la utani "Messi wa Chuga", wakimlinganisha na gwiji wa soka duniani, Lionel Messi.
Safari yake ya soka ilianza katika Future Stars Academy, ambako kipaji chake kilianza kuonekana mapema. Akiwa na umri wa miaka 12 pekee, alinasa macho ya maskauti wa Fountain Gate FC kupitia mashindano ya Chipukizi Cup, na kujiunga na klabu hiyo ili kuendeleza ndoto zake.
Baada ya kupandishwa kwenye kikosi cha wakubwa cha Fountain Gate FC, Chuga Boy aliangaza katika msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2025/26. Uwezo wake ulimfanya atwae tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi Oktoba 2025, baada ya kufunga mabao mawili na kuwa mmoja wa wachezaji waliovutia zaidi katika ligi.
Kiwango chake kiliwavutia maskauti kutoka klabu mbalimbali barani Afrika na Ulaya, jambo lililothibitisha ukubwa wa kipaji chake na mustakabali wake katika soka la kimataifa.
Mbali na mafanikio yake ya ngazi ya klabu, Juma Abushiri pia aliitumikia Timu ya Taifa ya Tanzania U-17 (Serengeti Boys), akiwa pia kwenye kikosi cha timu ya Taifa U20.
Yanga imemsajili Chuga Boy akiwa kwenye mchakato wa kuelekea Ubelgiji kufanya majaribio klabu ya KAA Genk, Wananchi wakapita nae kabla ya safari yake ambayo ilipangwa Julai 12 2026.
Bila shaka Yanga itampa jukwaa kubwa zaidi la kuonekana na kumuongezea thamani zaidi.