Mpaka sasa Yanga imetambulisha usajili wa nyota watatu wa ndani, ukiwa ni usajili wa kimkakati zaidi.
Baada ya kupitia kwenye changamoto kubwa msimu uliopita kutokana na uchovu uliochangiwa kwa kiasi kikubwa na ufinyu wa kikosi, Rais wa Yanga Injinia Hersi Said amerudi sokoni safari hii akifanya usajili wa kimkakati zaidi.
Usajili huo una lengo la kujenga Yanga nyingine itakayotawala soka la Tanzania kwa miaka mingi ijayo.
Mpaka sasa nyota waliosajiliwa bado ni vijana wadogo ambao watakuwa na muda mrefu wa kuwatumikia mabingwa hao wa soka Tanzania Bara.
Winga Juma Abushiri 'Chuga Boy' (18) na mshambuliaji Hussein Mihambo (19) hizi ni sajili za malengo ya muda mrefu huku Abdulnassir Assa Muhamed 'Gamal' (27) ukiwa ni usajili wa kuongeza nguvu safu ya ulinzi upande wa kulia akichukua nafasi iliyoachwa na Israel Mwenda.
Yanga pia imemsajili beki wa kati Mohamed Mussa (22) ambaye anasubiri utambulisho pia akitokea klabu ya Mashujaa Fc ukiwa usajili mwingine wa kimkakati.
Upande wa winga, Yanga pia imemuongeza Erick Mwijage (24) ambaye msimu uliopita aliitumikia klabu ya KMC.
Lakini pia kama haitoshi, Yanga inahusishwa na kiungo Alphonce Mabula (23) ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'.
Ikumbukwe pale Jangwani Yanga inaendelea kuwajenga nyota wengine chipukizi kama beki Aboubacar Nidhar 'Ninju' (18) na Abdulnassir Mohamed Abdallah ''Casemiro' (21).
Uongozi wa Yanga umekuwa na mkakati uliowazi, kujenga timu ya baadae itakayobebwa na wachezaji wa ndani, huku pia wakiimarisha kikosi kwa ajili ya ushindani wa sasa.
Yanga imefanikiwa kuwabakisha nyota wake muhimu ambao mikataba yao imemalizika huku pia ikitarajiwa kuongeza wachezaji wengine wenye uzoefu hasa kwa mashindano ya CAF.
Katika dirisha hili kuna mchanganyiko wa wachezaji, imefanyika 'scouting' kubaini vipaji vya ndani lakini pia kuongeza mastaa ambao tayari wana uzoefu ili kuhakikisha kunakuwa na uwiano kwenye kikosi.