Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema leo watakamilisha utambulisho wa wachezaji wa ndani waliosajiliwa na mabingwa hao wa soka Tanzania Bara.
Kunzia siku ya kesho Alhamisi, utambulisho wa nyota wa kigeni maalum kwa ajili ya mashindano ya Kimataifa utaanza.
"Leo tutafunga usajili wa bunduki za ndani tulizoziongeza kwenye kikosi chetu kwa ajili ya Msimu ujao. Halafu kuanzia Kesho tutaaanza kufungua boksi lenye silaha zetu hatari za Kimataifa. Natamani kweli kuwaambia hilo balaa ndugu zangu sema ndio hivyo siku hizi Simu yangu ameizuia Injinia. Napewa kuwasalimia halafu wanaichukua tena," alitamba Kamwe.
Yanga leo huenda ikafunga usajili wa wachezaji wa ndani kwa kuwatambulisha winga Erick Mwijage kutoka KMC na kiungo kinda Suleiman Mbarouk 'Mpemba D' kutoka JKU.
Mpaka sasa Yanga imetambulisha usajili wa wachezaji wanne wa ndani ambao ni Juma Abushiri 'Chuga Boya' (Fountain Gate), Hussein Juma Mihambo, Abdulnasir Gamal na Mohamed Mussa wote kutoka klabu ya Mashujaa Fc.