Wiki iliyopita winga wa zamani wa Yanga Skudu Makudubela alitangaza kustaafu soka baada ya takribani miaka 17 ya kucheza soka la ushindani.
Fundi huyo wa kuchezea mpira hakuchukua muda mrefu kupata ajira mpya, kwani ametangazwa kujiunga na klabu ya US Monastir ya Tunisia kama 'performance Analyst'
US Monastir inanolewa na kocha wa zamani wa Yanga Romain Folz ambaye msimu uliopita alikuwa kocha wa Yanga kwa takribani miezi mitatu kabla ya kupewa mkono wa kwaheri na nafasi yake kuchukuliwa na Pedro Goncalves.
Folz na Skudu waliwahi kufanya kazi pamoja kwenye klabu ya Marumo Gallants wakati huo Folz akiwa sehemu ya benchi la ufundi la timu hiyo.
Katika mahojiano maalum yaliyochapishwa na KickOff, Folz alibainisha kuwa alikiona kipaji cha Skudu kwenye uchambuzi na kumshauru achukue mafunzo ya ukocha.
Skudu tayari amehitimu mafunzo ya ngazi mbalimbali za ukocha na sasa atakuwa na nafasi ya kuhudumu kama mchambuzi katika klabu ya Monastir.
Afrika Kusini imeendelea kushamiri kwa kutoa makocha na wataalam wengi ambao sasa wanasambaa kila kona ya Afrika.
Hapa Tanzania benchi la ufundi la Yanga linaongozwa na kocha raia wa Afrika Kusini Manqoba Mngqithi akitua nchini na wataalam wengine kutoka Afrika Kusini. Awali Yanga ilihusishwa na Fadlu Davids kabla ya kumuajiri Manqoba.
Hata watani zao Simba nao wananolewa na kocha raia wa Afrika Kusini, Steve Barker nae akiwa na benchi linalojumuisha wataalum kutoka nchini humo.
Hivi karibuni klabu ya Pyramids Fc nayo ilimtangaza Rulani Mokwena kuwa kocha mkuu akitua kunako timu hiyo akitokea Al Ittihad ya Libya.
Mokwema amewahi kufanya kazi na Manqoba katika klabu ya Mamelodi Sundows ambayo pia iliwatoa makocha kama Folz, Mokwena na wengine katika benchi ambalo liliongozwa na Pitso Mosimane.
Manqoba alidumu Sundowns kwa kipindi cha miaka 11 bila shaka utaalam na uzoefu wake unakwenda kuleta mabadiliko makubwa kwa Yanga hasa kwenye michuano ya Ligi ya mabingwa.