Jana klabu ya Wiliete Sports Club ya Angola ilithibitisha kumsajili kiungo mshambuliaji wa Yanga Buba Jammeh. Buba amejiunga na timu hiyo kama mchezaji huru akisaini mkataba wa mwaka mmoja.
Winga huyo ambaye alijiunga na Yanga mwezi Januari kwenye usajili wa dirisha dogo hakuweza kuwashawishi mabosi wa mabingwa hao wa nchi.
Inaelezwa makubaliano ya pande mbili kusitisha mkataba kati yake na Yanga yalifikiwa na hivyo mchezaji huyo kuondoka akiwa huru.

Buba ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni ambao Yanga imefikia uamuzi wa kuachana nao kwenye dirisha hili.
Wachezaji wengine wa kigeni ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi cha Wananchi msimu ujao ni pamoja na Chadrack Boka, Lassine Kouma na Prince Dube ambaye tayari amerejea kwao Zimbabwe.
Pia yumo beki Frank Assink aliyerejea kwa waajiri wake Singida BS baada ya mkataba wa mkopo wa msimu mzima kumalizika.
Kiungo mshambuliaji Pacome Zouzoua yeye hatajumuishwa kwenye usajili akiendelea na mtibabu ya jeraha kubwa la mguu alilopata kwenye mchezo wa mwisho msimu uliopita dhidi ya JKT Tanzania.
Wachezaji wa kigeni ambao wana uhakika wa kusalia kwenye kikosi cha Yanga msimu ujao ni Djigui Diarra, Yao Kouassi, Maxi Nzengeli, Duke Abuya, Allan Okello na Laurindo Aurellio 'Depu'