Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, klabu ya Yanga, wameendelea kutikisa soko la usajili usiku wa kuamia leo wakimtambulisha mshambuliaji hatari, Cheikh Ibrahima Touré, raia wa Senegal mwenye uraia pacha wa Ufaransa.
Touré (29) anatua Jangwani akitokea klabu ya Al-Jabalain FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Saudi Arabia, ambako amesaini mkataba wa miaka miwili utakaomuweka klabuni hapo hadi mwaka 2028.
Usajili huu unatajwa kama mkakati wa Yanga kuongeza makali kwenye safu yao ya ushambuliaji kuelekea michuano ya ndani na ile ya kimataifa.
Mashine ya Mabao
Mshambuliaji huyo mwenye kimo cha mita 1.87 anasifika kwa uwezo wake mkubwa wa kutumia miguu yote miwili na umaliziaji wa hali ya juu uwanjani.
Takwimu zake za hivi karibuni zimekuwa chachu kubwa kwa viongozi wa Yanga kukimbilia saini yake ili kuimarisha eneo la umaliziaji.
Katika msimu uliopita wa 2025/2026 akiwa na Al-Jabalain nchini Saudi Arabia, Touré alikuwa mwiba mchungu kwa mabeki baada ya kucheka na nyavu mara 19 na kutoa pasi za mabao (asisti) 5 katika mashindano yote aliyocheza.
Kabla ya kutimkia Mashariki ya Kati, nyota huyo alijizolea sifa tele nchini Ufaransa ambako alicheza katika vilabu tofauti vya madaraja ya chini na kuacha alama ya ufungaji.
Akiwa na klabu ya AS Poissy, Touré alionyesha uwezo wa juu kwa kufunga jumla ya mabao 37, huku akitwaa kiatu cha mfungaji bora wa ligi katika mmoja wa misimu yake klabuni hapo.
Mbali na Poissy, takwimu zake katika klabu nyingine nchini Ufaransa zinaonyesha alifunga mabao 9 akiwa na Paris, 13 Atletico, mabao 11 akiwa na timu ya akiba ya Nancy-Lorraine, pamoja na mabao mengine kadhaa alipozitumikia klabu za Bergerac Périgord na Dijon FCO B.
Kwa jumla, mshambuliaji huyo anajiunga na Yanga akiwa na hazina ya mabao zaidi ya 85 kwenye soka la ushindani.
Matarajio ya Mashabiki
Kuwasili kwa Touré kumepokelewa kwa hisia chanya na mashabiki wa klabu hiyo ambao wanaamini ujio wake utaimarisha kikosi hicho kinacholenga kutetea ubingwa wa ndani na kufika mbali zaidi katika Michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika (CAFCL).
Wachambuzi wa soka wanamtaja Touré kama mchezaji mwenye uzoefu mkubwa wa mechi za shinikizo kubwa ambao utaisaidia timu hiyo kupata matokeo ya haraka.