Yanga yatuma ujumbe mzito: Uwekezaji mkubwa kwenye mabao msimu ujao

Shabiki NambaMoja By Shabiki NambaMoja
β€’
26 Jul 2026
Yanga yatuma ujumbe mzito: Uwekezaji mkubwa kwenye mabao msimu ujao

Baada ya kumaliza msimu uliopita huku safu ya ushambuliaji ikionekana kukosa makali katika baadhi ya mechi, Yanga imeamua kubadili mkakati wake.

Katika dirisha hili la usajili, mabingwa hao wa Tanzania wamewekeza nguvu kubwa kwenye eneo la ushambuliaji kwa lengo la kuhakikisha timu inakuwa na uwezo mkubwa wa kufunga na kutengeneza mabao msimu wa 2026/27.

Ibrahima Toure ametua na takwimu za kutisha

Kuondoka kwa Prince Dube hakujawa mwisho wa nguvu ya Yanga mbele ya lango. Wananchi wamemsajili mshambuliaji mwenye uzoefu mkubwa, Cheikh Ibrahima Toure, mzaliwa wa Senegal mwenye uraia wa Ufaransa.

Toure anatua akiwa na rekodi ya kuvutia baada ya kucheza katika klabu mbalimbali barani Ulaya na Mashariki ya Kati. Katika mechi 222 alizocheza, amefunga mabao 90 na kutoa pasi 32 za mabao, takwimu zinazoonyesha uwezo wake wa kuwa tegemeo katika safu ya ushambuliaji.

Depu aendelea kupewa imani

Mbali na Toure, Yanga imeamua kuendelea kumwamini Laurindo Aurelio "Depu". Mshambuliaji huyo alisajiliwa dirisha dogo la msimu uliopita na licha ya kusumbuliwa na majeraha yaliyompunguzia nafasi ya kucheza mara kwa mara, aliweza kuonyesha ubora wake.

Depu alifunga mabao tisa katika Ligi Kuu Tanzania Bara, akaongeza matatu kwenye Kombe la CRDB pamoja na mawili katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Takwimu hizo zimemfanya uongozi wa Yanga kuona bado ana mchango mkubwa kwa timu.

Justice Figuareido nae atajwa

Kana kwamba haitoshi, taarifa zinaeleza kuwa Yanga imekamilisha usajili wa mshambuliaji Justice Figuareido kutoka Eswatini, aliyekuwa akikichezea Chippa United ya Afrika Kusini.

Figuareido ni pendekezo la kocha Manqoba Mangqithi, msimu uliopita aling'ara na kikosi cha Chippa United akitoa pasi tano za mabao mabao huku akifunga mabao mawili. Akiwa na timu ya Taifa ya Eswatini, aliifungia mabao mawili kwenye kampeni ya kuwania tiketi ya michuano ya kombe la Dunia iliyofika tamati wiki iliyopita kwa Hispania kutwaa ubingwa.

Mzize anarejea

Habari nyingine njema kwa Wananchi ni kurejea kwa Clement Mzize, ambaye amekuwa nje kwa muda kutokana na majeraha.

Mzize ameanza kufanya mazoezi katika kambi ya maandalizi ya msimu mpya inayofanyika Avic Town, sambamba na beki Dickson Job. Ingawa bado wako chini ya uangalizi wa madaktari, kurejea kwao kunaongeza matumaini ya kuimarika kwa kikosi kabla ya msimu kuanza.

Wapishi wa mabao wameongezwa

Yanga haijawekeza kwa washambuliaji pekee. Pia imeimarisha safu ya viungo na mawinga kwa kusajili wachezaji wenye uwezo wa kutengeneza nafasi na kutoa pasi za mwisho.

Miongoni mwao ni Albert Kangwanda, aliyekuwa MVP wa Ligi Kuu Zambia msimu uliopita, pamoja na winga wa kimataifa wa Comoros, Housseine Zakouani.

Kwa upande wa wachezaji wa ndani, Juma Abushiri "Chuga Boy" na Erick Mwijage wameongezwa ili kuongeza ubunifu na kasi katika maeneo ya pembeni.

Aziz Ki bado ni lengo

Wakati huo huo, Yanga inaendelea kupambana kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki.

Taarifa zinaeleza kuwa Aziz Ki ameomba kuondoka Al Ittihad, huku klabu hiyo ikihitaji takribani Sh bilioni 1.9 ili kumruhusu. Kiungo huyo ameonekana akiendelea na mazoezi binafsi nchini, jambo linaloongeza tetesi kuwa dili hilo linaweza kukamilika katika siku zijazo.

Iwapo Yanga itafanikiwa kumrejesha Aziz Ki, itakuwa imeongeza mchezaji mwingine mwenye uwezo mkubwa wa kufunga na kutengeneza mabao. Hivi sasa Allan Okello ndiye namba 10 asilia pekee anayebeba jukumu hilo, hivyo kurejea kwa Aziz Ki kutaimarisha ushindani na kuongeza ubora katika eneo hilo muhimu.

Kwa kuangalia usajili uliofanywa hadi sasa, ni wazi Yanga imeamua kuwekeza kwenye mabao. Kuanzia kwa washambuliaji wa kati hadi mawinga na viungo washambuliaji, kila eneo limeongezewa ubora kwa lengo la kurejesha makali yaliyopungua msimu uliopita.

Iwapo wachezaji wapya wataendana haraka na mfumo wa kocha Mangqithi huku waliokuwepo wakiendelea na kiwango chao, Yanga inaweza kuwa moja ya timu zenye safu kali zaidi ya ushambuliaji katika msimu ujao, ikiwa na uwezo wa kupambana kwa mafanikio kwenye Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho na michuano ya CAF.

ADVERTISE HERE

Yanga SC Stories

Dladla alia na umaliziaji Yanga licha ya ushindi dhidi ya Mashujaa FC
Dladla alia na umaliziaji Yanga licha ya ushindi dhidi ya Mashujaa FC
1h ago
READ MORE β†’
Highlights: Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
Highlights: Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
2h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumatano, Oktoba 28 2026
Magazeti ya leo Jumatano, Oktoba 28 2026
2h ago
READ MORE β†’
FT : Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
FT : Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
12h ago
READ MORE β†’
Magoli; Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
Magoli; Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
12h ago
READ MORE β†’
Kikosi : Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
Kikosi : Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
15h ago
READ MORE β†’
Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
20h ago
READ MORE β†’
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
23h ago
READ MORE β†’
Yanga inahitaji utulivu, si vita ya lawama
Yanga inahitaji utulivu, si vita ya lawama
1d ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
1d ago
READ MORE β†’